Mkristo
lazima atoe zaka? HIli ni swali ambalo limewasumbua wengi, ni swali
ambalo wakati mwingine majibu yake huambatana na vitisho, na shuku
kwamba muulizaji anaroho ya kutokutii maandiko. Walio wengi ujua kuwa
ni lazima mkristo atoe zaka na kutoitoa husababisha laana maishani. Kutokana na kuogopa laana wengi wao hutoa si kwa kupenda na kwa furaha
bali kwa maumivu yasiyokifani, na mara nyingi hutoa kwa kusitasita na
kuruka ruka, hata kuwafanya wapokeaji kutunga sheria au taratibu
zitakazo wabana watoaji waweze kulitoa kwa shuruti hata kama hawapendi.
Wengine wamekwenda mbali zaidi kuwanyima washirika wengine msaada wawapo
katika vipindi vigumu kama kufiwa au kuugua kwa sababu tu hawatoi zaka au kama
wanatoa hawatoi sawa sawa kulingana na rekodi zao.
Somo
hili linalenga kujibu swali hili kwa undani, likianza kwa kutoa
historia ya utoaji wa zaka katika Agano la Kale mpaka wakati wa Agano
Jipya. Katika somo hili utajifunza kuwa mkristo hafungwi na sheria ya
zaka na kwamba utoaji wa mkristo husukumwa na moyo wa furaha na ihari na
kwa kadri Mungu alivyo mbariki. Kwamba mkristo kwa kusukumwa na moyo
huo aweza hata kutoa zaidi ya fungu la kumi maadamu utoaji wake
haukuambatana na shuruti ya namna yoyote!
“Je,
mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mwaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema,
tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa
laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani,
ili kiwemo chakula cha katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema
BWANA wa majeshi…”
Katika maneno ya nabii Malaki
tunaona maneno mawili ya msingi yanajitokeza katika mashutumu ya Mungu kwa watu
wake Israeli kuhusu utoaji wao, maneno hayo ni “ZAKA” na “DHABIHU (SADAKA).”
ZAKA
Neno la Kiebrania ma’ser (zaka)
maana yake halisi ni “sehemu ya kumi.” Katika sheria ya Mungu wana wa Israeli
walitakiwa kutoa sehemu ya kumi ya mifugo yao, na mazao yao ya ardhi, pamoja na
mapato yao kama kama kutambua kwamba Mungu amewabariki. (Law 27:30-32; Hes
18:21,26; Kum 14:22-29). Zaka zilitolewa kuwategemeza Walawi (Hes 18:21) na
makuhani (Hes 18:28) katika kujipatia chakula kitakatifu (Kumb 14:22-27) na kwa
ajili ya kuwasaidia yatima na wajane (Kumb 14:28-29).
Ili dhana ya ZAKA ipate kueleweka
maneno yafuatayo yatolewe ufafanuzi kwanza; Sheria, Walawi, Makuhani, Madhabahu
na dhabihu.
Sheria
Sheria ni kanuni zilizowekwa na
mwenye mamlaka zinazoendesha taratibu za maisha ya watu au kikundi Fulani
husika, na ambazo ni lazima zifuatwe, kwenda kinyume nazo matokeo yake huwa ni
adhabu kali.
Katika Agano la Kale mtu
aliyeshindwa kwenda kama sheria ya Mungu ilivyoagiza alihesabika kuwa amelaaniwa
(Kumb 27:26; Gal 3:10; Zab 119:21; Yer 11:3). Hivyo ZAKA katika Agano la Kale
ilikuwa chini ya sheria ya Musa, kutoitoa kama sheria ilivyoagiza ilihesabika
kama kumwibia Mungu na matokeo yake ilikuwa ni kulaaniwa. (Mal 3).
Walawi
Hawa ni wana wa Lawi, mtoto wa
tatu wa Yakobo (Israeli). Israeli alizaa wana kumi na wawili; Reubeni, Simeoni,
Lawi, Yuda, Isakari, Zabuloni, Gadi, Asheri, Dani, Naftali, Yusufu na Benyamini
(Kut 1:1-5; Mwa 46:8-21). Wakiwa jangwani kuelekea nchi ya ahadi, Musa akiwa
anaongea na Mungu katika mlima Sinai, alipokawia huko, watu wakaasi (Kut
32:1-25), wakatengeneza sanamu na kuiabud, ndipo BWANA akamwambia Musa, “Haya
shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi
zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya
kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakisema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee
Israeli iliyokutoa katika nchi ya Misri.” Baada ya uasi wa wana wa Israeli,
wana wa Lawi peke yao ndio waliobaki upande wa BWANA. Siku ile Musa
alipotelemka kutoka mlimani na kukuta watu wameasi, alisimama katika mlango wa
marago, akasema, mtu awaye yote aliye upande wa BWANA, na aje kwangu. Wan wa
Lawi wote wakamkusanyikia (mst 25-28).
Baada ya kufanya aliyowaagiza
akawaambia, “jiwekeni wakfu kwa BWANA
leo, naam, kila mtu juu ya
mwanawe na juu ya ndugu yake; ili awape Baraka leo (mst 29). Tangu siku hiyo
wana wa Lawi wakachaguliwa kuwa watumishi wa BWANA. Kutokana na utumishi wao
ulivyokuwa, hawakupewa nchi ya kumiliki walipofika katika nchi ya ahadi bali
makabila mengine kumi na moja yaliyobaki aliamriwa kuwapa zaka kuwa urithi wao
(Hes 18;23,24; Heb 7:5) na miji katika nchi zao kwa ajili ya kuishi na kulisha
mifugo yao (Hes 35:1-8; Yos 21:1-3).
Hapo Mwanzo Mungu alikuwa
amejichukulia wa kwanza wa kiume wa binadamu na mnyama kuwa wake (Kut 13:2)
lakini baadae akalichukua kabila la Lawi kuwa badala ya wazaliwa wa kwanza na
wanyama wao kuwa badala ya wazaliwa wa kwanza wa wanyama wa wana wa Israeli
(Hes 3:12-45).
Kazi zao zilikuwa ni; kumtumikia
BWANA na kuwabarikia watu kwa jina lake
(Kumb 10:8), kuwatumikia makuhani (Hes 3:5-9), kuilinda hema (Hes 18:3,4),
kugawanya ZAKA (2Nya 31;11-19), kuandaa dhabihu kwa ajili ya makuhani (2Nya
35:10-14), kufundisha watu (2Nya 17:8-11), kutoa hukumu ya maamuzi (Kumb
17:9-11), kutoa ulinzi kwa mfalme (2Nya 23:2-10), kumwimbia Mungu (1Nya
25:1-7), na kulitangulia jeshi (2Nya 20:19-21,28). Ni kutokana na majukumu hayo
wana wa Israeli waliamriwa kuwapa ZAKA wana wa Lawi.
Makuhani
Neno heireus (Gk) ambalo
hutafsiriwa kuhani humaanisha mtu ambaye hutoa dhabihu na mwenye mamlaka juu ya
shughuli zote zihusianazo na mwenendo mzima wa shughuli husika. Tukiachana na kuongelea makuhani wa miungu
mingine, tuangalie makuhani wa Mungu aliye hai.
Ili mtu awe kuhani wa Mungu ilikuwa ni lazima atoke katika familia ya
Haruni (Kut. 29:9) nje na familia hiyo hapakuwepo kuhani katika wana wa Israeli
waliowahi kuwa makuhani nje na familia ya Haruni na kabla la Lawi ni wawili tu,
mfalme na kuhani Melkzedeki (Mwa 14:18, Ebr. 7:1-4, 6) ambaye hajulikani ukoo
wake (hana baba, hana mama, hana wazazi, hana Mwanzo wa siku zake, wala mwisho
wa uhai wake, bali amefananishwa na mwana wa Mungu), mwingine ni Yesu Kristo
(Ebr. 7:25-28) ambaye hutoka katika kabila la Yuda (Mw. 49:10 Luka 3:23 – 33)
Makuhani wa Mungu aliye hai walitakiwa kufanya yafutayo kati ya
wana wa Israeli, kutoa dhabihu(Law 1:1 -7) kutunza mahali patakatifu
(hema) (Hes 3:38),
kuhakikisha taa haizimiki daima katika hema (Kut 27:20-21) kutunza
moto katikamadhabahu usizimike daiam (Law 6:12-13). Kulifunika sanduku na vitu vyote
vya hema safari ilipoanza (Hesa 4:5-15), kufukiza uvumba (Kut
30:7,8),
kuwabariki watu (Hes 6:23-27), kuwatakaza (kuwapatanisha )
wenye unajisi
mbele za BWANA (Law 15;15-31), kubaini ukomo(Law 13:1-17), na
kufundisha
sharia (Law 10:11)
Makuhani walipokea ZAKA kutoka kwa Walawi. Sadaka hii
iliyotolewa na
Walawi kwa makuhani iliitwa sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA
(heave sacrifice)
fungu la kumi la mafungu ya kumi waliyopokea walawi kutoka kwa
wana wa
Israeli. (Hesa 18:28)
Makuhani (wa nyakati zote) wanaotambuliwa katika maandiko ni
kama hawa
wafutao, Wamegawanyika
katika makundi matatu:-
1. Makuhani kabla ya sharia
Hapa tunamuona
mmoja tu Mfalme na Kuhani mkuu Melkisedeki (Mw 14:18, Ebr 7:1)
2. Makuhani wa Mungu aliye hai wakati wa
sharia
Hawa wote wa
kipindi hiki walitoka katika familia ya Haruni, nje na hiyo kama tulivyojifunza
hapakuwepo kuhani, Nao ni kama wafutao, (1) Haruni (Kut 31:10), Abiathari (Sam
23:9) , Abimeleki (1Sam 22:11), amaria (2Ny 19:11), Anania (Mdo 23:2), Kayafa
(Mat. 26:3), Eliazari (Hesa 16:39), Eli (1Sam 1:9), Eliashibu (Neh 3:`1),
Ezekieli (Ezek 1:3), Ezra (Ezra 7:11, 12), Hilkia (2Fal 22:4), Yehoiada (2Fal
11:9), Yehozadaki (Hag 1:1), Yoshua (Zeka 3:1), Maaseya (Yer 37:3), Pashuri
(Yer 20:1), Fineasi (Yos 22:30), Skewa (Mdo 19:14), Seraya (2Fal 25:18),
Shelemiya (Neh 13:13), Uriya (2Fal 16:10), Zabudi 1Fal 4:5), Zakaria (Luka 1:5),
Zadoki (2Sam 15:27), Zefania (2Fal 25:18)
3. Makuhani katika kanisa la Agano Jipya
Katika wakati
wa Agano jopya Kristo ndiye anayetajwa kuwa ni kuhani Mkuu tena wa milele (Ebr
3:1) Kundi jingine linalotajwa kuwa makuhani ni wakristo wote wa kweli (Uf 1:5-6,
1Pet 2:9) Hatuoni majina maalumu ya kikundi cha watu maalumu waliofanywa
makuhani, hata Paulo mwenyewe hakuwahi kujiita kuhani wala mtume yeyote. Hivyo katika agano jipya Kristo pekee ndiye
kuhani Mkuu na haitaji msaidizi hapa duniani.
Kwa hiy kitendo cha mtu yeyote kujipa ukuhani maalum tofauti na ule wa
waumini wote ni kuidharau kazi ya Kristo na kuihubiri injili nyingine,
itakayomletea laana (Gal 1;6-9)
NAMNA TATU ZA UTOAJI NA ULAJI WA ZAKA
Zaka zilizotolewa ziliweza
kugawanywa katika makundi matatu.
Kundi la kwanza: ni lile la
zaka zilizotolewa kwa walawi peke yao wakati wote kwa ajili ya uhitaji wao wa
kila siku, ikizingatiwa kuwa hawakuwa na urithi pamoja na wana wa Israeli. Zaka hii huitwa Zaka ya walawi. Tena zaka
yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi ni ya BWANA, ni
takatifu kwa BWANA (Law 27:30), Tena zaka yote ya Ng’ombe au ya kondoo kila
apitaye chini ya fimbo; sehemu ya kumi watakuwa ni watakatifu kwa BWANA. (Mst
32) Kwa kuwa zaka ya wana wa Israeli, waisongezayo kuwa sadaka ya kuinuliwa kwa
BWANA nimewapa Walawi kuwa urithi wao;
kwa hiyo nimewaambia, ya kwamba katika wana wa Israeli hawwtakuwa na urithi
uwao wote (Hesa 18:24). Baada ya
kuipokea hii Walawi walitakiwa kutoa nao fungul la kumi kwa makuhani (Hesa 18:28)
Aina ya pili: ni ile
tunayoweza kuiita ZAKA YA SIKUKUU (festival tithe) zaka hii uliliwa na wana wa
Israeli wote pamoja na walawi kama sherehe.
Na BWANA aliwachagulia sehemu ya kwenda kuilia. Kama sehemu hiyo ilikuwa mbali walitakiwa
kuiuza zaka wakapata fedha ndizo wakasafiri nazo, pindi wakifika huko wanunue
tena vitu ili wavitumie katika siku hiyo maalum. Ebu tusome maandiko haya, ‘Usikose kutoa zaka
ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokanayo shambani mwaka
baada ya mwaka.
Nawe utakula mbele za
BWANA Mungu wako. Mahali atakapochagua apakalishe jina lake, zaka ya nafaka
zako, na divai yako, na mafuta yako, na wazaliwa wa kwanza kwa makundi yako ya
ng’ombe na kondoo, ili upate kujifunza kumcha BWANA Mungu wako daima, na njia kiwa
ndefu mno nawe, usiweze kuzichukua kwa kuwa mahali ni mbali nawe mno utakapo
chagua BWANA, Mungu wako apakalishe jina lake, hapo atakapokubarikia BWANA,
Mungu wako; ndipo azibadili ziwe fedha na kufunga zie fedha uende nazo mkononi
mwako, hata mahali atakapochagua BWANA Mungu wako, na zie fedha zitumie kwa
chochote itakachotamani roho yako, ng’ombe au kondoo au divai, au kileo, au
roho yako itakacho kwako chochote nawe
utakula huko mbele za BWANA Mungu wako, tena furahi wewe na nyumba yako, na
Mlaw aliye ndani ya malango yako usimwache, kwani hana fungu wala urithi pamoja
nawe (Kumb 14:22-7).
Aina ya tatu: ni ile
inayoweza kuitwa zaka ya ustawi au
zaka za huduma kwa makundi maalumu katika jamii, mfano watoto yatima, wajane na
wageni, Itakumbukwa kuwa hata Walawi nao walikuwa ni kundi maalum, hivyo katika
zaka zote (namba mbili na tatu) hawakukosa kupewa. Aina hii ya utoaji zaka ilifanyika kila mwisho
wa mwaka wa tatu. Na ilikuwa ni zaka ya
mapato yote ya mwaka huo mzima (Kumb 14:28-29) mwaka huu uliitwa mwaka wa
kutolea zaka (Kumb 26:12).
Katika maandiko yetu ya msingi wa
somo hili yanayotoka katika kitabu cha Malaki yanatuonesha kuwa Mungu hakuwa
anawakemea wana wa Israeli kwa suala la ZAKA tu bali pia alitaja na DHABIHU kwamba nayo ilikuwa haitolewi
sawasawa (Mal 1:8), walitoa sadaka waliovipofu, walio vilema na wagonjwa. Katika sura ya pili (mst 9) makuhani
waliadhibiwa na Mungu kwa kufundisha sharia isivyopasa kwa kupendelea watu
katika sheria. Neno Dhabihu lina
uhusiano wa moja kwa moja na neno MADHABAHU (Altar) Neno la Kigriki
thusiasterion linalomaanisha madhabahu hutokana na neno thusiazo lenye maana ya
‘kutoa kafara’ Kamusi ya Kiswahili sanifu.
BIBLIA YA MAFUZO YA UZIMA TELE UK. 314
inaeleza maana ya neno kafara kuwa ni ‘kitu chochote kinachotolewa kuwa ni
sadaka kwa Mwenyezi Mungu au kwa mizimu ili kuepuka balaa. Madhara na maafa,
tambiko, dhabihu’ Madhabahu ni sehemu
maalum iliyojengwa kwa mawe na udongo kama ilivyokuwa desturi ya wana wa
Israeli iliyotumika kutolea kafara (dhabihu)
Maana ya neno dhabihu ni kitu kilichotolewa sadaka au mnyama
aliyechinjwa kwa ajili ya sadaka kwa hiyo DHABIHU na MADHABAHU ni kama pande
mbili za shilingi ambazo huwezi kuzitenganisha.
Haiwezi kuwepo dhabihu bila kuwepo na madhabahu, lakini pia
hapawezi
kuwepo vitu hivi viwili bila kuwepo KUHANI ambaye hufanya kazi ya kutoa
dhabihu juu ya madhabahu, lakini pia lazima kuwepo watu ambao kazi hiyo
inafanyika
kwa ajili yao.
AINA TANO ZA DHABIHU KATIKA AGANO LA KALE
Katika Agano la Kale zilikuwepo aina tano za dhabihu zilizotolewa
pale mtu alipotaka kuonesha shukrani kwa Mungu au alipotenda dhambi tena isiyo
ya kukusudia au kosa lolote ili kupatanishwa na Mungu. Dhabihu hizo ni kama zifuatazo:-
a) Sadaka
ya kuteketezwa (the burnt offering) (Law 1:1-17)
b) Sadaka
ya nafaka Grain Cereal Offering) (Law 2:1-16)
c) Sadaka
ya amani (the Peace Offering) (Law 3:1-17)
d) Sadaka
ya Dhambi (the Sin Offering) (Law 5:1-13)
e) Sadaka
ya Hatia/Sadaka ya malipizi (the Guilt Offeering )(Law 5:14-6:7)
Sadaka nyingine zilikuwa ni
sadaka ya hiari na sadaka ya nadhiri zilizotolewa kwa utashi wa mtu mwenyewe
bila kulazimishwa. Mfano mtu angeweza
kutoa nadhiri kwa Bwana bila kulazimishwa.
Isipokuwa alipokuwa ameisha itoa ilikuwa ni lazima atomize kama sivyo
kitendo hicho kilihesabika kuwa ni dhambi, na kama mtu aliamua kwa moyo wake
kutoa kama alivyoahiari au alivyoahidi, ilimlazimu kutoa sadaka iliyo kamilifu
(Hesa 30: Kumb 23;21-23; Law 22:18-26), kinyume na hapo alihesabiwa kuwa
katenda dhambi.
Tunapomalizia sehemu hii,
ikumbukwe kuwa ZAKA katika Agano la Kale ilikuwa si sadaka bali ilikuwa ni mali
ya BWANA mwenyewe na hivyo ilikuwa ni lazima kwa kila mwana wa Israeli,
hapakuwepo uhiari wowote katika kutoa fungu la kumi, kutokulitoa kulisababisha
laana. Kutoa zaka ilikuwa ni amri ya
Daima. Sadaka nyingne mfano sadaka ya
dhambi na hatia zilifata masharti ya kama mtu akitenda au kutokutenda dhambi,
kama mtu hakutenda dhambi au kosa lolote lilotaka kupatanishwa na Mungu wake
angeweza kukaa maisha yake yote bila kutoa sadaka hizo, japo haikuwa vyepesi
mtu kutokutenda dhambi.
Hivyo hizi
zilitolewa na mtu aliyekuwa katika hali ya kukosa, ndio maana maneno yote
yahusuyo sadaka hizi, huanza na maneno yenye kuonesha usharti hivi, ‘na mtu
yeyote akifanya dhambi…. Ndipo…’ nk ukichnguza ulazima wa sadaka hizo hapo juu
utaona kuwa haukuwa kama wa ZAKA.
Ulazima wa ZAKA ulikuwa mzito. Ni
kutokana na uzito huo, watu wasio na ujuzi wa neno la Mungu leo hudanganywa na
kutishwa na walimu wajanja kuwa wasipotoa ZAKA watalaaniwa, na hivyo kujikuta
wanawekwa chini ya sharia ya Agano la Kale kwa ujinga wao, na kurudishwa chini
ya laana na kuifanya kazi ya Kristo aliyoifanya miaka elfu mbili iliyopita ya
kuwatoa chini ya laana kuwa bure!
MASWALI YA MSINGI
1. Je
kwa kuwa ZAKA ilikuwa ni amri (shEria) ya daima kwa wana wa Israeli, Daima hiyo
ilikuwa inaenda mpaka wapi, ni mpaka mwisho wa Agano la kale au ilikuwa
inapenya mpaka Agano jipya yaani mpaka Yesu atakapo rudi mara ya pili?
2. Tumeona
kuwa zaka zilitolewa kwa Walawi ambao hawakuwa na urithi katika Israeli na kwa
makuhani na makundi maalumu kama watoto yatima, wajane na wageni, je, (a) Leo
kuna watu maalum wanaoitwa walawi katika kanisa la Agano jpya? (b) Leo
tunawanadamu ambao ni makuhani katika ukristo kutoka katika familia ya Haruni
kama shria iagizavyo? (c) Leo katika kanisa la Agano jipya makundi maalum
huweza kushriki katika kuyala mafungu ya kumi? (d) sikukuu ya zaka ambapo watu
wenyewe hukaa na kuila zaka wenyewe ipo katika utaratibu wa utoaji zaka katika
Agano jipya? (e) mwaka wa zaka huwa unaadhimishwa katika kanisa la Agano jipya?
Kama siyo kwa nini? (f) waweza kuyataja majina ya walawi na makuhani kama
yalivyoandikwa kwa mitume katika vitabu vya Agano jipya?
3. Katika
maandiko ya Malaki tumeona Mungu akiwashutumu wana wa Israeli kwa wizi wa mambo
mawili (1) Zaka (2) na Dhabihu. Je, (a)
Leo, dhabihu bado zinatolewa kwa kufuata sharia ya Musa iagizavyo au
zinatolewaje kiagano jipya? (b) kuna mahali dhabihu zilipokatazwa zisiendelee
kutolewa lakini mahali hapo au pengine pakaruhusu Zaka ziendelee kutolewa,
lakini bila kufuata sharia iliyokuwa inaongoza utoaji wake?
4. Mungu
anasema Katika Malaki, ‘Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika
nyumba yangu..’ Je, (a) Leo nyumba ya Bwana inayosemwa hapa iko wapi katika
Agano jpya? (b) Mungu bado anaishi katika nyumba zilizojengwa kwa mikono?
5. Biblia
inatwambia kuwa Kristo ndiye kuhani mkuu, Je, (a) ukuu wake unaupata kwa sababu
kuna makuhani wanadamu maalumu katika agano jipya ambapo yeye ni mkuu halafu
wao ni wadogo? Au ina maana gani kwani yeye kuitwa kuhani mkuu? (b)
kuna umuhimu bado wa kuwa na makuhani wengi kama ilivyokuwa kipindi cha
Agano la Kale, wakati neon linatuambia sababu ya kwa nini wale walikuwa ni
wengi, kwamba ;tena wale walifanywa makuhani wengi kwa sababu walizuiliwa na
mauti wasikae; bali yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka’
(Ebr 7:23-24) au anahitaji wasaidizi?
Majibu ya
maswali haya lazima yapatikane na kupimwa katika maandiko yaliyotumika kwa
uhalali, majibu yaliyo nje na maandiko au katika naandiko yaliyopindishwa
hutoka kwa yule mwovu!!
ZAKA NA UTOAJI KATIKA AGANO JIPYA
2Kor 9:6-8
“Lakini nasema neon hili, Apandanye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu
atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa
huzuni wala si kwa lazima maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa
ukunjufu”
ZAKA KATIKA AGANO JIPYA
Kama tulivyoona
katika sehemu ya kwanza ZAKA ni jambo zito kwani husababisha mtu
asiyezingatiaamri yake kulaaniwa (Mal).
Ni kutokana na uzito wake somo hili limeandikwa ili tupate kujifunza
habari zake na kama katika Agano Jipya kanisa linaagizwa kutoa zaka kama
ilivyokuwa katika Agano la kale?
Katika vitabu
vya agano Jipya zaka imetajwa mara nane tu. Katika vitabu vitatu tu, Mathayo
(23:23), Luka 11:42;18:12), Waebrania (7:5,6,8,9). Ebu tuyapitie moja baada ya
jingine tuone kama yana amri kwa kanisa kuhusu utoaji zaka.
Mathayo (23:23) ‘Ole wenu waandishi na
mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira. Lakini
mmeacha mambo makuu ya sharia, yaani, adili na rehema, na imani, hayo imewapasa
kuyafanya, wala yale mengine msiyaache’
Luka (18:12)’Mimi nafunga mara mbili
kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote’
Waebrania (7:5) ‘Na katika wana wa Lawi
nao, wale waupatao ukuhani, wana amri kutwaa sehemu ya kumi kwa watu wao,
yaani, ndugu zao, kwa agano la sharia, ijapokuwa wametoka katika viuno vya
Ibrahimu.’
Waebrania (7:6) ‘Bali yeye, ambaye
uzazi wake haukuhesabiwa kuwa umetoka kwa hao, alitwaa sehemu ya kumi kwa
Ibrahimu, akambariki yeye aliye na ile ahadi.’
Waebrania (7:8) ‘Na hapa wanadamu
wapatikanao na kufa hutwaa sehemu ya kumi, bali huko yeye ashuhudiwaye kwamba
yu hai’
Waebrania (7:9) ‘Tena yaweza kusemwa ya
kuwa, kwa njia ya Ibrahimu, hata Lawi apokeaye sehemu ya kumi alitoa sehemu ya
kumi.’
Ukiyachunguza
kwa umakini maandiko hayo ya pekee kuhusu ZAKA katika vitabu vya AGano Jipya,
utagundua kuwa hakuna neno hata moja linaloagiza waumini wa Agano Jipya kuendelea kushika sharia ya Zaka . Katika Mathayo na Luka tunaona Yesu akiongea
na waandishi na Mafarisayo ambao ama kwa hakika walikuwa chini ya sheria na
iliyokuwa inawaagiza na kwamba walitakiwa kuiangalia sharia nzima na sio zakat
u jambo ambalo lilionekana kusisitizwa sana kuliko mambo ya msingi. Haya maneno hayakuwahusu wanafunzi wake, wala
kwamba
(1)
mafundisho hayo hulenga kuwarudisha waliokwisha
komb olewa katika Vifungo vya sharia na hivyo kuwaweka chini ya sharia, na kwa
kuwa wote walio wa matendo ya sharia wamelaaniwa kwa sababu hawawezi kuitimiza
sharia yote basi hawa nao tayari wamelaaniwa.
(2)
Kwa mafundisho hayo wameidharau kazi nzito ya
ukombozi aliyoifanya Bwana Yesu pale msalabani, na hivyo kuwaletea uharibifu
wanaowafundisha na wao pia.
Ebu sasa
tuangalie toaji kama unavyofundishwa katika Agano Jipya.
UTOAJI KATIKA KANISA LA AGANO JIPYA
Kuna mahali
pengi katika Agano jipya ambapo Wakristo wanaagizwa kutoa, lakini hawajaagizwa
ni kiasi gani au asilimia ngapi watoe.
Sasa hebu tuone jinsi ambavyo biblia inafundisha utoaji wa Mkristo
(ambaye ayko chini ya sheria bali chini ya neema) unavyotakiwa kuwa.
Sura (8,9) kuu
mbili zifundishazo utoaji wa Mkristo zinapatikana katika kitabu cha Wakorintho
wa pili, Kila mwanafunzi wa Yesu lazima azisome kwa makini ilia pate kujifunza
kuhusu utoaji katika kanisa.
Utoaji katika
Agano Jipya ni kama sadaka ya hiari ya Agano la Kale, Mkristo halazimishwi
kutoa, bali hutakiwa kutoa kutoka moyoni mwake, Neno linasema hivi, ‘Kila mtu
na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima;
maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu’ (2kor 9:7)
Je, ni kiasi gani Mkristo anatakiwa kutoa?
Ebu tuangalie
mfano ufuatao kutoka (2Korintho 8:1-5)
“Tena ndugu
zangu twawaarifu habari ya neema ya Mungu waliyopewa makanisa ya makedonia;
maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na
umasikini wao ulikuwa mwingi ulio waongezea utajiri wa ukarimu wao. Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na
zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; wakituomba sana
pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia
watakatifu. Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza
walijitoa nafsi kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu.”
Katika mstari
wa 5 tunasoma kuwa, … bali kwanza walijitoa nafsi kwa Bwana… ‘Hili ndilo jambo
la msingi sana kuliko ni kiasi gani tutoacho Warumi (12:1) hukubaliana na
mstari huu, ‘Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili
yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu
yenye maana ‘Mungu hutaka nia na maisha ya mtu mwenyewe. Kumtolea Mungu zawadi za fedha wakati mioyo
yetu haiku sawa naye haifaidii kitu.
Mstari wa 2
unasema, ‘….umasikini wao uliokuwa
mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao.’ Walitoa kwa ukarimu bila
kujali umasikini waliokuwa nao! ‘wingi
wa furaha yao…’ walikuwa naraha katika kutoa kwao na walifanya hivyo kwa
furaha yao …’ walikuwa na raha katika kutoa kwao na walifanya hivyo kwa
furaha ‘….kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao’ (mst 3) walitoa kwa jinsi
walivyoweza na zaidi, walijinyima nafsi zao ili kutoa zaidi. Utoaji huu ulikuwa ni utoaji wa kujitoa
dhabihu. ‘Kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao’ (Mst 3) huu unaonesha kuwa hawakushurutishwa katika kutoa kwao, walitoa kwa moyo wa kupenda.
Ni utoaji wa namna hii ambao mkristo anatakiwa kuufuata na ndio utoaji wa ki-maandiko.
Means Mkristo hapashwi kutowa zaka?
ReplyDeletenimejifunza sana kwenye somo hili hapa juu, sijui hawa watumishi wa Mungu wanayajua haya kwa namna hii au wamejaa ghiliba na uizi!!, maana sheria wanaikamata hapa tu kwenye fungu la kumi na sio fungu la kumi lote kama maandiko yasemavyo bali kama wanaonavyo inafaa wao. maana kwa mjibu wa uchambuzi huu mafungu ya kumi yapo matatu.
ReplyDeletenaomba nipate ufafanuzi, wana wa Israel walitoa fedha zao? dhahabu na silver? na je utoaji wao ulikua kwa mwezi, kwa juma au kwa utaratibu upi?
kwa leo ni haya tu
Bwana Yesu apewe sifa sana. Mimi shida naona hipo apa, tujaribu kutafautisha HIZI(AGANO) 2. Tukielewa tafauti ya hizi Agano ,bitakuwa birahisi sana. Agano la kale (TORATI),Agano Jipia(NEEMA).Tunaamini yakuwa Yesu ametungikwa musalabani kwa ajili atupe neema, manayake TORATI imeshaa kwisha, TORATI imekuwa ni kivuli ki nayo tuleta kwa YESU. Na YESU KRISTO wakati amekuwa pale musalabani, ametangaza kwamba YOTE yamekwisha.Kwamucango wangu,maswala yakutowa; naamini katika AGANO JIPIA siyo sheria. Tumepewa rohomutakatifu ili atuongoze katika kweli yote. Katika AGANO JIPIA ,tuko wana wa MUNGU, ca BABA ni cetu, na CETU ni ca BABA.kwa mufano kama TUKIMUPEYA BABA 1\10 ,kwa kweli tutakuwa wa coyo sana.Tutakuwa bado hatujabarikiwa kabisa,.Hatutowi ili,tubarikiwe,tayari tumeshaabarikIwa,tuko wana MUNGU na warisi, YESU KRISTO amelipa garama zote . kwa hiyo, tusome taratibu yamaandiko kwakutafautisha maagano ma wili, JE WEWE UNAISHI KATIKA AGANO GANI? LAKALE AO JIPIA??????????
ReplyDelete