Wednesday, 17 July 2013

Wakristo na utoaji zaka katika Agano Jipya

Mkristo lazima atoe zaka? HIli ni swali ambalo limewasumbua wengi, ni swali ambalo wakati mwingine majibu yake huambatana na vitisho, na shuku kwamba muulizaji anaroho ya kutokutii maandiko. Walio wengi ujua kuwa ni lazima mkristo atoe zaka na kutoitoa husababisha laana maishani. Kutokana na kuogopa laana wengi wao hutoa si kwa kupenda na kwa furaha bali kwa maumivu yasiyokifani, na mara nyingi hutoa kwa kusitasita na kuruka ruka, hata kuwafanya wapokeaji kutunga sheria au taratibu zitakazo wabana watoaji waweze kulitoa kwa shuruti hata kama hawapendi. Wengine wamekwenda mbali zaidi kuwanyima washirika wengine msaada wawapo katika vipindi vigumu kama kufiwa au kuugua kwa sababu tu hawatoi zaka au kama wanatoa hawatoi sawa sawa kulingana na rekodi zao. 



Somo hili linalenga kujibu swali hili kwa undani, likianza kwa kutoa historia ya utoaji wa zaka katika Agano la Kale mpaka wakati wa Agano Jipya. Katika somo hili utajifunza kuwa mkristo hafungwi na sheria ya zaka na kwamba utoaji wa mkristo husukumwa na moyo wa furaha na ihari na kwa kadri Mungu alivyo mbariki. Kwamba mkristo kwa kusukumwa na moyo huo aweza hata kutoa zaidi ya fungu la kumi maadamu utoaji wake haukuambatana na shuruti ya namna yoyote!





“Je, mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mwaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula cha katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi…”

Katika maneno ya nabii Malaki tunaona maneno mawili ya msingi yanajitokeza katika mashutumu ya Mungu kwa watu wake Israeli kuhusu utoaji wao, maneno hayo ni “ZAKA” na “DHABIHU (SADAKA).”

ZAKA
Neno la Kiebrania ma’ser (zaka) maana yake halisi ni “sehemu ya kumi.” Katika sheria ya Mungu wana wa Israeli walitakiwa kutoa sehemu ya kumi ya mifugo yao, na mazao yao ya ardhi, pamoja na mapato yao kama kama kutambua kwamba Mungu amewabariki. (Law 27:30-32; Hes 18:21,26; Kum 14:22-29). Zaka zilitolewa kuwategemeza Walawi (Hes 18:21) na makuhani (Hes 18:28) katika kujipatia chakula kitakatifu (Kumb 14:22-27) na kwa ajili ya kuwasaidia yatima na wajane (Kumb 14:28-29).

Ili dhana ya ZAKA ipate kueleweka maneno yafuatayo yatolewe ufafanuzi kwanza; Sheria, Walawi, Makuhani, Madhabahu na dhabihu.

Sheria
Sheria ni kanuni zilizowekwa na mwenye mamlaka zinazoendesha taratibu za maisha ya watu au kikundi Fulani husika, na ambazo ni lazima zifuatwe, kwenda kinyume nazo matokeo yake huwa ni adhabu kali.
Katika Agano la Kale mtu aliyeshindwa kwenda kama sheria ya Mungu ilivyoagiza alihesabika kuwa amelaaniwa (Kumb 27:26; Gal 3:10; Zab 119:21; Yer 11:3). Hivyo ZAKA katika Agano la Kale ilikuwa chini ya sheria ya Musa, kutoitoa kama sheria ilivyoagiza ilihesabika kama kumwibia Mungu na matokeo yake ilikuwa ni kulaaniwa. (Mal 3).

Walawi
Hawa ni wana wa Lawi, mtoto wa tatu wa Yakobo (Israeli). Israeli alizaa wana kumi na wawili; Reubeni, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Zabuloni, Gadi, Asheri, Dani, Naftali, Yusufu na Benyamini (Kut 1:1-5; Mwa 46:8-21). Wakiwa jangwani kuelekea nchi ya ahadi, Musa akiwa anaongea na Mungu katika mlima Sinai, alipokawia huko, watu wakaasi (Kut 32:1-25), wakatengeneza sanamu na kuiabud, ndipo BWANA akamwambia Musa, “Haya shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakisema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli iliyokutoa katika nchi ya Misri.” Baada ya uasi wa wana wa Israeli, wana wa Lawi peke yao ndio waliobaki upande wa BWANA. Siku ile Musa alipotelemka kutoka mlimani na kukuta watu wameasi, alisimama katika mlango wa marago, akasema, mtu awaye yote aliye upande wa BWANA, na aje kwangu. Wan wa Lawi wote wakamkusanyikia (mst 25-28).

Baada ya kufanya aliyowaagiza akawaambia, “jiwekeni wakfu kwa BWANA  leo, naam, kila  mtu juu ya mwanawe na juu ya ndugu yake; ili awape Baraka leo (mst 29). Tangu siku hiyo wana wa Lawi wakachaguliwa kuwa watumishi wa BWANA. Kutokana na utumishi wao ulivyokuwa, hawakupewa nchi ya kumiliki walipofika katika nchi ya ahadi bali makabila mengine kumi na moja yaliyobaki aliamriwa kuwapa zaka kuwa urithi wao (Hes 18;23,24; Heb 7:5) na miji katika nchi zao kwa ajili ya kuishi na kulisha mifugo yao (Hes 35:1-8; Yos 21:1-3). 

Hapo Mwanzo Mungu alikuwa amejichukulia wa kwanza wa kiume wa binadamu na mnyama kuwa wake (Kut 13:2) lakini baadae akalichukua kabila la Lawi kuwa badala ya wazaliwa wa kwanza na wanyama wao kuwa badala ya wazaliwa wa kwanza wa wanyama wa wana wa Israeli (Hes 3:12-45).
Kazi zao zilikuwa ni; kumtumikia BWANA  na kuwabarikia watu kwa jina lake (Kumb 10:8), kuwatumikia makuhani (Hes 3:5-9), kuilinda hema (Hes 18:3,4), kugawanya ZAKA (2Nya 31;11-19), kuandaa dhabihu kwa ajili ya makuhani (2Nya 35:10-14), kufundisha watu (2Nya 17:8-11), kutoa hukumu ya maamuzi (Kumb 17:9-11), kutoa ulinzi kwa mfalme (2Nya 23:2-10), kumwimbia Mungu (1Nya 25:1-7), na kulitangulia jeshi (2Nya 20:19-21,28). Ni kutokana na majukumu hayo wana wa Israeli waliamriwa kuwapa ZAKA wana wa Lawi.

Makuhani
Neno heireus (Gk) ambalo hutafsiriwa kuhani humaanisha mtu ambaye hutoa dhabihu na mwenye mamlaka juu ya shughuli zote zihusianazo na mwenendo mzima wa shughuli husika.  Tukiachana na kuongelea makuhani wa miungu mingine, tuangalie makuhani wa Mungu aliye hai.  Ili mtu awe kuhani wa Mungu ilikuwa ni lazima atoke katika familia ya Haruni (Kut. 29:9) nje na familia hiyo hapakuwepo kuhani katika wana wa Israeli waliowahi kuwa makuhani nje na familia ya Haruni na kabla la Lawi ni wawili tu, mfalme na kuhani Melkzedeki (Mwa 14:18, Ebr. 7:1-4, 6) ambaye hajulikani ukoo wake (hana baba, hana mama, hana wazazi, hana Mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na mwana wa Mungu), mwingine ni Yesu Kristo (Ebr. 7:25-28) ambaye hutoka katika kabila la Yuda (Mw. 49:10 Luka 3:23 – 33)

Makuhani wa Mungu aliye hai walitakiwa kufanya yafutayo kati ya wana wa Israeli, kutoa dhabihu(Law 1:1 -7) kutunza mahali patakatifu (hema) (Hes 3:38),
kuhakikisha taa haizimiki daima katika hema (Kut 27:20-21) kutunza moto katikamadhabahu usizimike daiam (Law 6:12-13).  Kulifunika sanduku na vitu vyote
vya hema safari ilipoanza (Hesa 4:5-15), kufukiza uvumba (Kut 30:7,8),
kuwabariki watu (Hes 6:23-27), kuwatakaza (kuwapatanisha ) wenye unajisi
mbele za BWANA (Law 15;15-31), kubaini ukomo(Law 13:1-17), na kufundisha
sharia (Law 10:11)

Makuhani walipokea ZAKA kutoka kwa Walawi. Sadaka hii iliyotolewa na
Walawi kwa makuhani iliitwa sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA (heave sacrifice)
fungu la kumi la mafungu ya kumi waliyopokea walawi kutoka kwa wana wa
Israeli. (Hesa 18:28)

Makuhani (wa nyakati zote) wanaotambuliwa katika maandiko ni kama hawa
wafutao,  Wamegawanyika katika makundi matatu:-
1.     Makuhani kabla ya sharia
Hapa tunamuona mmoja tu Mfalme na Kuhani mkuu Melkisedeki (Mw 14:18, Ebr 7:1)

2.     Makuhani wa Mungu aliye hai wakati wa sharia
Hawa wote wa kipindi hiki walitoka katika familia ya Haruni, nje na hiyo kama tulivyojifunza hapakuwepo kuhani, Nao ni kama wafutao, (1) Haruni (Kut 31:10), Abiathari (Sam 23:9) , Abimeleki (1Sam 22:11), amaria (2Ny 19:11), Anania (Mdo 23:2), Kayafa (Mat. 26:3), Eliazari (Hesa 16:39), Eli (1Sam 1:9), Eliashibu (Neh 3:`1), Ezekieli (Ezek 1:3), Ezra (Ezra 7:11, 12), Hilkia (2Fal 22:4), Yehoiada (2Fal 11:9), Yehozadaki (Hag 1:1), Yoshua (Zeka 3:1), Maaseya (Yer 37:3), Pashuri (Yer 20:1), Fineasi (Yos 22:30), Skewa (Mdo 19:14), Seraya (2Fal 25:18), Shelemiya (Neh 13:13), Uriya (2Fal 16:10), Zabudi 1Fal 4:5), Zakaria (Luka 1:5), Zadoki (2Sam 15:27), Zefania (2Fal 25:18)

3.     Makuhani katika kanisa la Agano Jipya
Katika wakati wa Agano jopya Kristo ndiye anayetajwa kuwa ni kuhani Mkuu tena wa milele (Ebr 3:1) Kundi jingine linalotajwa kuwa makuhani ni wakristo wote wa kweli (Uf 1:5-6, 1Pet 2:9) Hatuoni majina maalumu ya kikundi cha watu maalumu waliofanywa makuhani, hata Paulo mwenyewe hakuwahi kujiita kuhani wala mtume yeyote.  Hivyo katika agano jipya Kristo pekee ndiye kuhani Mkuu na haitaji msaidizi hapa duniani.  Kwa hiy kitendo cha mtu yeyote kujipa ukuhani maalum tofauti na ule wa waumini wote ni kuidharau kazi ya Kristo na kuihubiri injili nyingine, itakayomletea laana (Gal 1;6-9)

NAMNA TATU ZA UTOAJI NA ULAJI WA ZAKA
Zaka zilizotolewa ziliweza kugawanywa katika makundi matatu.
Kundi la kwanza:  ni lile la zaka zilizotolewa kwa walawi peke yao wakati wote kwa ajili ya uhitaji wao wa kila siku, ikizingatiwa kuwa hawakuwa na urithi pamoja na wana wa Israeli.  Zaka hii huitwa Zaka ya walawi.  Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi ni ya BWANA, ni takatifu kwa BWANA (Law 27:30), Tena zaka yote ya Ng’ombe au ya kondoo kila apitaye chini ya fimbo; sehemu ya kumi watakuwa ni watakatifu kwa BWANA. (Mst 32) Kwa kuwa zaka ya wana wa Israeli, waisongezayo kuwa sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA nimewapa Walawi kuwa urithi  wao; kwa hiyo nimewaambia, ya kwamba katika wana wa Israeli hawwtakuwa na urithi uwao wote (Hesa 18:24).   Baada ya kuipokea hii Walawi walitakiwa kutoa nao fungul la kumi kwa makuhani (Hesa 18:28)

Aina ya pili:  ni ile tunayoweza kuiita ZAKA YA SIKUKUU (festival tithe) zaka hii uliliwa na wana wa Israeli wote pamoja na walawi kama sherehe.  Na BWANA aliwachagulia sehemu ya kwenda kuilia.  Kama sehemu hiyo ilikuwa mbali walitakiwa kuiuza zaka wakapata fedha ndizo wakasafiri nazo, pindi wakifika huko wanunue tena vitu ili wavitumie katika siku hiyo maalum.  Ebu tusome maandiko haya, ‘Usikose kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokanayo shambani mwaka baada ya mwaka.  

 Nawe utakula mbele za BWANA Mungu wako. Mahali atakapochagua apakalishe jina lake, zaka ya nafaka zako, na divai yako, na mafuta yako, na wazaliwa wa kwanza kwa makundi yako ya ng’ombe na kondoo, ili upate kujifunza kumcha BWANA Mungu wako daima, na njia kiwa ndefu mno nawe, usiweze kuzichukua kwa kuwa mahali ni mbali nawe mno utakapo chagua BWANA, Mungu wako apakalishe jina lake, hapo atakapokubarikia BWANA, Mungu wako; ndipo azibadili ziwe fedha na kufunga zie fedha uende nazo mkononi mwako, hata mahali atakapochagua BWANA Mungu wako, na zie fedha zitumie kwa chochote itakachotamani roho yako, ng’ombe au kondoo au divai, au kileo, au roho yako itakacho  kwako chochote nawe utakula huko mbele za BWANA Mungu wako, tena furahi wewe na nyumba yako, na Mlaw aliye ndani ya malango yako usimwache, kwani hana fungu wala urithi pamoja nawe (Kumb 14:22-7).

Aina ya tatu:  ni ile inayoweza kuitwa zaka ya ustawi au zaka za huduma kwa makundi maalumu katika jamii, mfano watoto yatima, wajane na wageni, Itakumbukwa kuwa hata Walawi nao walikuwa ni kundi maalum, hivyo katika zaka zote (namba mbili na tatu) hawakukosa kupewa.  Aina hii ya utoaji zaka ilifanyika kila mwisho wa mwaka wa tatu.  Na ilikuwa ni zaka ya mapato yote ya mwaka huo mzima (Kumb 14:28-29) mwaka huu uliitwa mwaka wa kutolea zaka (Kumb 26:12).
 
Katika maandiko yetu ya msingi wa somo hili yanayotoka katika kitabu cha Malaki yanatuonesha kuwa Mungu hakuwa anawakemea wana wa Israeli kwa suala la ZAKA tu bali pia alitaja na DHABIHU kwamba nayo ilikuwa haitolewi sawasawa (Mal 1:8), walitoa sadaka waliovipofu, walio vilema na wagonjwa.  Katika sura ya pili (mst 9) makuhani waliadhibiwa na Mungu kwa kufundisha sharia isivyopasa kwa kupendelea watu katika sheria.  Neno Dhabihu lina uhusiano wa moja kwa moja na neno MADHABAHU (Altar) Neno la Kigriki thusiasterion linalomaanisha madhabahu hutokana na neno thusiazo lenye maana ya ‘kutoa kafara’ Kamusi ya Kiswahili sanifu.

BIBLIA YA MAFUZO YA UZIMA TELE UK. 314 inaeleza maana ya neno kafara kuwa ni ‘kitu chochote kinachotolewa kuwa ni sadaka kwa Mwenyezi Mungu au kwa mizimu ili kuepuka balaa. Madhara na maafa, tambiko, dhabihu’  Madhabahu ni sehemu maalum iliyojengwa kwa mawe na udongo kama ilivyokuwa desturi ya wana wa Israeli iliyotumika kutolea kafara (dhabihu)  Maana ya neno dhabihu ni kitu kilichotolewa sadaka au mnyama aliyechinjwa kwa ajili ya sadaka kwa hiyo DHABIHU na MADHABAHU ni kama pande mbili za shilingi ambazo huwezi kuzitenganisha.  Haiwezi kuwepo dhabihu bila kuwepo na madhabahu, lakini pia hapawezi kuwepo vitu hivi viwili bila kuwepo KUHANI ambaye hufanya kazi ya kutoa dhabihu juu ya madhabahu, lakini pia lazima kuwepo watu ambao kazi hiyo inafanyika kwa ajili yao. 

 AINA TANO ZA DHABIHU KATIKA AGANO LA KALE
Katika Agano la Kale zilikuwepo aina tano za dhabihu zilizotolewa pale mtu alipotaka kuonesha shukrani kwa Mungu au alipotenda dhambi tena isiyo ya kukusudia au kosa lolote ili kupatanishwa na Mungu.  Dhabihu hizo ni kama zifuatazo:-
a)     Sadaka ya kuteketezwa (the burnt offering) (Law 1:1-17)
b)     Sadaka ya nafaka Grain Cereal Offering) (Law 2:1-16)
c)      Sadaka ya amani (the Peace Offering) (Law 3:1-17)
d)     Sadaka ya Dhambi (the Sin Offering) (Law 5:1-13)
e)     Sadaka ya Hatia/Sadaka ya malipizi (the Guilt Offeering )(Law 5:14-6:7)

Sadaka nyingine zilikuwa ni sadaka ya hiari na sadaka ya nadhiri zilizotolewa kwa utashi wa mtu mwenyewe bila kulazimishwa.  Mfano mtu angeweza kutoa nadhiri kwa Bwana bila kulazimishwa.  Isipokuwa alipokuwa ameisha itoa ilikuwa ni lazima atomize kama sivyo kitendo hicho kilihesabika kuwa ni dhambi, na kama mtu aliamua kwa moyo wake kutoa kama alivyoahiari au alivyoahidi, ilimlazimu kutoa sadaka iliyo kamilifu (Hesa 30: Kumb 23;21-23; Law 22:18-26), kinyume na hapo alihesabiwa kuwa katenda dhambi.

Tunapomalizia sehemu hii, ikumbukwe kuwa ZAKA katika Agano la Kale ilikuwa si sadaka bali ilikuwa ni mali ya BWANA mwenyewe na hivyo ilikuwa ni lazima kwa kila mwana wa Israeli, hapakuwepo uhiari wowote katika kutoa fungu la kumi, kutokulitoa kulisababisha laana.  Kutoa zaka ilikuwa ni amri ya Daima.  Sadaka nyingne mfano sadaka ya dhambi na hatia zilifata masharti ya kama mtu akitenda au kutokutenda dhambi, kama mtu hakutenda dhambi au kosa lolote lilotaka kupatanishwa na Mungu wake angeweza kukaa maisha yake yote bila kutoa sadaka hizo, japo haikuwa vyepesi mtu kutokutenda dhambi. 

 Hivyo hizi zilitolewa na mtu aliyekuwa katika hali ya kukosa, ndio maana maneno yote yahusuyo sadaka hizi, huanza na maneno yenye kuonesha usharti hivi, ‘na mtu yeyote akifanya dhambi…. Ndipo…’ nk ukichnguza ulazima wa sadaka hizo hapo juu utaona kuwa haukuwa kama wa ZAKA.  Ulazima wa ZAKA ulikuwa mzito.  Ni kutokana na uzito huo, watu wasio na ujuzi wa neno la Mungu leo hudanganywa na kutishwa na walimu wajanja kuwa wasipotoa ZAKA watalaaniwa, na hivyo kujikuta wanawekwa chini ya sharia ya Agano la Kale kwa ujinga wao, na kurudishwa chini ya laana na kuifanya kazi ya Kristo aliyoifanya miaka elfu mbili iliyopita ya kuwatoa chini ya laana kuwa bure!

MASWALI YA MSINGI
1.      Je kwa kuwa ZAKA ilikuwa ni amri (shEria) ya daima kwa wana wa Israeli, Daima hiyo ilikuwa inaenda mpaka wapi, ni mpaka mwisho wa Agano la kale au ilikuwa inapenya mpaka Agano jipya yaani mpaka Yesu atakapo rudi mara ya pili?

2.      Tumeona kuwa zaka zilitolewa kwa Walawi ambao hawakuwa na urithi katika Israeli na kwa makuhani na makundi maalumu kama watoto yatima, wajane na wageni, je, (a) Leo kuna watu maalum wanaoitwa walawi katika kanisa la Agano jpya? (b) Leo tunawanadamu ambao ni makuhani katika ukristo kutoka katika familia ya Haruni kama shria iagizavyo? (c) Leo katika kanisa la Agano jipya makundi maalum huweza kushriki katika kuyala mafungu ya kumi? (d) sikukuu ya zaka ambapo watu wenyewe hukaa na kuila zaka wenyewe ipo katika utaratibu wa utoaji zaka katika Agano jipya? (e) mwaka wa zaka huwa unaadhimishwa katika kanisa la Agano jipya? Kama siyo kwa nini? (f) waweza kuyataja majina ya walawi na makuhani kama yalivyoandikwa kwa mitume katika vitabu vya Agano jipya?

3.      Katika maandiko ya Malaki tumeona Mungu akiwashutumu wana wa Israeli kwa wizi wa mambo mawili (1) Zaka (2) na Dhabihu.  Je, (a) Leo, dhabihu bado zinatolewa kwa kufuata sharia ya Musa iagizavyo au zinatolewaje kiagano jipya? (b) kuna mahali dhabihu zilipokatazwa zisiendelee kutolewa lakini mahali hapo au pengine pakaruhusu Zaka ziendelee kutolewa, lakini bila kufuata sharia iliyokuwa inaongoza utoaji wake?

4.      Mungu anasema Katika Malaki, ‘Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu..’ Je, (a) Leo nyumba ya Bwana inayosemwa hapa iko wapi katika Agano jpya? (b) Mungu bado anaishi katika nyumba zilizojengwa kwa mikono?

5.      Biblia inatwambia kuwa Kristo ndiye kuhani mkuu, Je, (a) ukuu wake unaupata kwa sababu kuna makuhani wanadamu maalumu katika agano jipya ambapo yeye ni mkuu halafu wao ni wadogo? Au ina maana gani kwani yeye kuitwa kuhani mkuu?  (b)  kuna umuhimu bado wa kuwa na makuhani wengi kama ilivyokuwa kipindi cha Agano la Kale, wakati neon linatuambia sababu ya kwa nini wale walikuwa ni wengi, kwamba ;tena wale walifanywa makuhani wengi kwa sababu walizuiliwa na mauti wasikae; bali yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka’ (Ebr 7:23-24) au anahitaji wasaidizi?

Majibu ya maswali haya lazima yapatikane na kupimwa katika maandiko yaliyotumika kwa uhalali, majibu yaliyo nje na maandiko au katika naandiko yaliyopindishwa hutoka kwa yule mwovu!!

ZAKA NA UTOAJI KATIKA AGANO JIPYA
2Kor 9:6-8 “Lakini nasema neon hili, Apandanye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni wala si kwa lazima maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu”

ZAKA KATIKA AGANO JIPYA
Kama tulivyoona katika sehemu ya kwanza ZAKA ni jambo zito kwani husababisha mtu asiyezingatiaamri yake kulaaniwa (Mal).  Ni kutokana na uzito wake somo hili limeandikwa ili tupate kujifunza habari zake na kama katika Agano Jipya kanisa linaagizwa kutoa zaka kama ilivyokuwa katika Agano la kale?

Katika vitabu vya agano Jipya zaka imetajwa mara nane tu. Katika vitabu vitatu tu, Mathayo (23:23), Luka 11:42;18:12), Waebrania (7:5,6,8,9). Ebu tuyapitie moja baada ya jingine tuone kama yana amri kwa kanisa kuhusu utoaji zaka.

Mathayo (23:23) ‘Ole wenu waandishi na mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira. Lakini mmeacha mambo makuu ya sharia, yaani, adili na rehema, na imani, hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache’

Luka (18:12)’Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote’
Waebrania (7:5) ‘Na katika wana wa Lawi nao, wale waupatao ukuhani, wana amri kutwaa sehemu ya kumi kwa watu wao, yaani, ndugu zao, kwa agano la sharia, ijapokuwa wametoka katika viuno vya Ibrahimu.’

Waebrania (7:6) ‘Bali yeye, ambaye uzazi wake haukuhesabiwa kuwa umetoka kwa hao, alitwaa sehemu ya kumi kwa Ibrahimu, akambariki yeye aliye na ile ahadi.’

Waebrania (7:8) ‘Na hapa wanadamu wapatikanao na kufa hutwaa sehemu ya kumi, bali huko yeye ashuhudiwaye kwamba yu hai’

Waebrania (7:9) ‘Tena yaweza kusemwa ya kuwa, kwa njia ya Ibrahimu, hata Lawi apokeaye sehemu ya kumi alitoa sehemu ya kumi.’

Ukiyachunguza kwa umakini maandiko hayo ya pekee kuhusu ZAKA katika vitabu vya AGano Jipya, utagundua kuwa hakuna neno hata moja linaloagiza waumini wa Agano Jipya  kuendelea kushika sharia ya Zaka .  Katika Mathayo na Luka tunaona Yesu akiongea na waandishi na Mafarisayo ambao ama kwa hakika walikuwa chini ya sheria na iliyokuwa inawaagiza na kwamba walitakiwa kuiangalia sharia nzima na sio zakat u jambo ambalo lilionekana kusisitizwa sana kuliko mambo ya msingi.  Haya maneno hayakuwahusu wanafunzi wake, wala kwamba

(1)   mafundisho hayo hulenga kuwarudisha waliokwisha komb olewa katika Vifungo vya sharia na hivyo kuwaweka chini ya sharia, na kwa kuwa wote walio wa matendo ya sharia wamelaaniwa kwa sababu hawawezi kuitimiza sharia yote basi hawa nao tayari wamelaaniwa.

(2)   Kwa mafundisho hayo wameidharau kazi nzito ya ukombozi aliyoifanya Bwana Yesu pale msalabani, na hivyo kuwaletea uharibifu wanaowafundisha na wao pia.
Ebu sasa tuangalie toaji kama unavyofundishwa katika Agano Jipya.

UTOAJI KATIKA KANISA LA AGANO JIPYA
Kuna mahali pengi katika Agano jipya ambapo Wakristo wanaagizwa kutoa, lakini hawajaagizwa ni kiasi gani au asilimia ngapi watoe.  Sasa hebu tuone jinsi ambavyo biblia inafundisha utoaji wa Mkristo (ambaye ayko chini ya sheria bali chini ya neema) unavyotakiwa kuwa.

Sura (8,9) kuu mbili zifundishazo utoaji wa Mkristo zinapatikana katika kitabu cha Wakorintho wa pili, Kila mwanafunzi wa Yesu lazima azisome kwa makini ilia pate kujifunza kuhusu utoaji katika kanisa.

Utoaji katika Agano Jipya ni kama sadaka ya hiari ya Agano la Kale, Mkristo halazimishwi kutoa, bali hutakiwa kutoa kutoka moyoni mwake, Neno linasema hivi, ‘Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu’ (2kor 9:7)

Je, ni kiasi gani Mkristo anatakiwa kutoa?
Ebu tuangalie mfano ufuatao kutoka (2Korintho 8:1-5)
“Tena ndugu zangu twawaarifu habari ya neema ya Mungu waliyopewa makanisa ya makedonia; maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umasikini wao ulikuwa mwingi ulio waongezea utajiri wa ukarimu wao.  Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu. Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu.”

Katika mstari wa 5 tunasoma kuwa, … bali kwanza walijitoa nafsi kwa Bwana… ‘Hili ndilo jambo la msingi sana kuliko ni kiasi gani tutoacho Warumi (12:1) hukubaliana na mstari huu, ‘Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana ‘Mungu hutaka nia na maisha ya mtu mwenyewe.  Kumtolea Mungu zawadi za fedha wakati mioyo yetu haiku sawa naye haifaidii kitu.

Mstari wa 2 unasema, ‘….umasikini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao.’ Walitoa kwa ukarimu bila kujali umasikini waliokuwa nao! ‘wingi wa furaha yao…’ walikuwa naraha katika kutoa kwao na walifanya hivyo kwa furaha yao …’ walikuwa na raha katika kutoa kwao na walifanya hivyo kwa furaha  ‘….kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao’ (mst 3) walitoa kwa jinsi walivyoweza na zaidi, walijinyima nafsi zao ili kutoa zaidi.  Utoaji huu ulikuwa ni utoaji wa kujitoa dhabihu.  Kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao’ (Mst 3) huu unaonesha kuwa hawakushurutishwa katika kutoa kwao, walitoa kwa moyo wa kupenda.

Ni utoaji wa namna hii ambao mkristo anatakiwa kuufuata na ndio utoaji wa ki-maandiko.

3 comments:

  1. Means Mkristo hapashwi kutowa zaka?

    ReplyDelete
  2. nimejifunza sana kwenye somo hili hapa juu, sijui hawa watumishi wa Mungu wanayajua haya kwa namna hii au wamejaa ghiliba na uizi!!, maana sheria wanaikamata hapa tu kwenye fungu la kumi na sio fungu la kumi lote kama maandiko yasemavyo bali kama wanaonavyo inafaa wao. maana kwa mjibu wa uchambuzi huu mafungu ya kumi yapo matatu.
    naomba nipate ufafanuzi, wana wa Israel walitoa fedha zao? dhahabu na silver? na je utoaji wao ulikua kwa mwezi, kwa juma au kwa utaratibu upi?
    kwa leo ni haya tu

    ReplyDelete
  3. Bwana Yesu apewe sifa sana. Mimi shida naona hipo apa, tujaribu kutafautisha HIZI(AGANO) 2. Tukielewa tafauti ya hizi Agano ,bitakuwa birahisi sana. Agano la kale (TORATI),Agano Jipia(NEEMA).Tunaamini yakuwa Yesu ametungikwa musalabani kwa ajili atupe neema, manayake TORATI imeshaa kwisha, TORATI imekuwa ni kivuli ki nayo tuleta kwa YESU. Na YESU KRISTO wakati amekuwa pale musalabani, ametangaza kwamba YOTE yamekwisha.Kwamucango wangu,maswala yakutowa; naamini katika AGANO JIPIA siyo sheria. Tumepewa rohomutakatifu ili atuongoze katika kweli yote. Katika AGANO JIPIA ,tuko wana wa MUNGU, ca BABA ni cetu, na CETU ni ca BABA.kwa mufano kama TUKIMUPEYA BABA 1\10 ,kwa kweli tutakuwa wa coyo sana.Tutakuwa bado hatujabarikiwa kabisa,.Hatutowi ili,tubarikiwe,tayari tumeshaabarikIwa,tuko wana MUNGU na warisi, YESU KRISTO amelipa garama zote . kwa hiyo, tusome taratibu yamaandiko kwakutafautisha maagano ma wili, JE WEWE UNAISHI KATIKA AGANO GANI? LAKALE AO JIPIA??????????

    ReplyDelete